30 Okt 2013

Tahadhari kuhusu watoto wa miujiza UK



Gilbert Deya anayetakikana na serikali ya Kenya kwa tuhuma za kuwaiba watoto yuko Uingereza 

Mashirika matatu nchini uingereza yamewatahadharisha wafanyakazi wa jamii kuhusu wanandoa wanaosema wanakwenda Afrika kwa matibabuili waweze kutungishwa mimba na kupata mtoto wa kimiujiza na kisha baadaye kurejea Uingereza wakiwa na mtoto.

Mara nyingi mtoto huyo huwa sio mwanao halisi.

Mashirika hayo yanasema kuwa visa vya kile kinachojulikana kama watoto wa miujiza, ni biashara haramu ya kuwauza watoto.

Katika moja ya visa hivyo, Mke na mumewe waliosema kuwa walikuwa na tatizo la kupata mtoto walikwenda kwa kile walichosema ni matibabu nchini Nigeria na kutokana na imani yao ya kikristo waliweza kupata mtoto wa miujiza.

Baada ya kufanyiwa uchunguzi, iligunduliwa kuwa mtoto huyo hakuwa wao kama walivyokuwa wamedai na hivyo serikali kumchukua mtoto huyo kumtunza.

Angalau visa vingine vinne vya mama kupata mtoto kwa muujiza vimechunguzwa na maafisa mjini London na hata baadhi kufikishwa mahakamani London.

Visa vingine kumi na viwili viligunduliwa katika ubalozi wa Uingereza mjini Lagos, Nigeria, ingawa maafisa wanasema kuwa huenda ni vingi kuliko idadi hiyo.

Ushauri huu umetolewa na mashirika matatu ya kushungulikia maslahi ya watoto.


Yanasema kuwa wafanyakazi wa jamii lazima wahusishe polisi ambao wanaweza kuchunguza ikiwa watu wengine wamehusika na sakata hiyo au vitendo vingine vya uhalifu au hata vitendo vya udanganyifu.

Kashfa hii pia iliwahi kusikika Kenya baada ya mhubiri Gilbert Deya aliyekimbilia Uingereza kudai kuwa ana uwezo wa kuwatungisha mimba kina mama kimiujiza kupitia maombi.

Gilbert Deya, ambaye huongoza misa katika eneo la Peckham London Kusini, amekuwa akikabiliana kisheria asirejeshwe Kenya tangu mwaka 2007, akidai kuwa hatua yeyote ile itakayochukuliwa dhidi yake itakiuka haki zake za kibinadamu.

Serikali ya Kenya inadai kuwa aliwaiba watoto watano kati ya mwaka 1999 na mwaka 2004.

Wanawake ambao hawangeweza kutunga mimba ama waliokuwa wamepita umri wa kuzaa, waumini katika kanisa lake la Peckham Kusini mwa London waliahidiwa wataweza kupata watoto kimiujiza.

Lakini watoto hao walikuwa wanazaliwa katika zahanati bandia mjini Nairobi nchini Kenya.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni